Milioni 60 zabadili maisha ya madereva bajaji Mbalizi

0
54

Viongozi na wanachama wa kikundi cha Vijana Waendesha Bajaji (VIWABA) eneo la Mbalizi, Wilaya ya Mbeya wamesema kuwa mkopo wa zaidi ya TZS milioni 60 walioupata kutoka halmashauri umewawezesha kujiajiri sambamba kujikwamua kimaisha.

Katibu wa Viwaba, Anangisye Jengela alisema hayo jana wakati akieleza mafanikio na uwepo wa mikopo ya halmashauri ambayo imekuwa msaada kwa wananchi mbalimbali. Alisema Viwaba ilianza na mtaji wa Sh1 milioni, kisha wakapanda hadi kupata Sh6 milioni lakini malengo yao hayakutimia.

“Mwaka jana tuliweza kukopeshwa Sh60.7 milioni na halmashauri kupitia mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na halmashauri. Baada ya kupata mkopo ule tuliutumia kununua bajaji kwa sababu wengi wa vijana wa hapa walikuwa wameajiriwa kuendesha bajaji za watu, binafsi,” alisema Jengela.

Jengela alisema kupitia mkopo huo, vijana wa Viwaba wameweza kujiajiri na kujiendesha kimaisha bila kutegemea ajira kutoka kwa watu binafsi au Serikalini. Alisema mbali na hilo, Viwaba imejikita kwenye kilimo cha alizeti baada ya kununua shamba la ekari moja.

Mkopo huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali lililowataka wakurugenzi wa manispaa, majiji na halmashauri mbalimbali nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Mipango yetu ya baadaye kuanzisha kiwanda cha kuzalisha alizeti ambacho kikikamilika kitatoa fursa ya ajira kwa vijana wengi zaidi. Tumeshaanza kulima alizeti, lakini tukifanikiwa kupata eneo tutafanya kilimo kikubwa kitakachoajiri vijana wengi,” alisema Jengela.

Send this to a friend