Miradi ya UVIKO19 ilivyowatoa vijana mitaani na kuwapa ajira

0
27

Utekelezaji wa miradi mbalimbali kupitia fedha za UVIKO19 kwa kutumia mafundi wa ndani hasa wanaoshi eneo ambako mradi unafanyika limepongezwa na wananchi kutokana na kutoa fursa za ajira kwa makundi mbalimbali.

Mkazi wa Mtama, Shodadi  Katuya ambaye ni fundi sanifu ni miongoni mwa wanaufaika wakubwa wa utekelezaji wa mradi wa kituo cha afya cha Mtama kilichogharimu takribani TZS milioni 250.

Amesema ujenzi wa kituo cha afya cha Mtama umefungua ajira nyingi kwa vijana pamoja na mama lishe waliokuwa wakipeleka vyakula kwa mafundi waliokuwa wakijenga kituo hicho cha afya ambacho kipo mbioni kukamilika.

“Kuna vijana wengi wameacha kuzurura mtaani, wamepata vibarua katika ujenzi huu. Msimu wa kilimo watu wameachana na kilimo cha jembe la mkono, badala yake wamewekeza kwenye matrekta baada ya kupata fedha kwenye vibarua,” amesema Katuya.

Ameongeza kuwa kutokana na malipo waliyoyapata, baadhi ya vijana wameweza kuwekeza katika kilimo kuanzia ekari tatu hadi nne za mashamba, huku wakiendelea na shughuli hizo za ujenzi.

“Wengine wameweza kujikimu na kuwanunulia sare za shule watoto na ndugu zao hasa wakati wa msimu kufungua shule. Mfano mimi hivi sasa namiliki pikipiki yangu binafsi kutokana na ujenzi huu,” amesema fundi huyo.

Shania Makota mkazi wa Narungombe wilayani Ruangwa, anayejishughulisha biashara ya mama lishe amesema mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha eneo hilo, umemsaidia kwa kiasi kikubwa kwa sababu alikuwa anajipatia fedha baada ya kuwauzia chakula mafundi.

“Nimekuwa nikiwaletea chakula tangu wanachimba msingi hadi sasa hatua ya umaliziaji. Nimenufaika kwa kiasi kikubwa kwa sababu nina wadogo zangu wanakwenda shule kupitia shughuli hii, mradi umenifanya niweze kumudu gharama za maisha,” amesema Shania.

Alisema kupitia fedha anazozipata katika shughuli hiyo, anafirikia kununua kiwanja ndani ya mwezi huu kwa ajili ya kuanza mchakato wa ujenzi, huku akiendelea kuwasomesha wadogo zake watatu pamoja na kuwalea wazazi wake.

Send this to a friend