Mita za maji za malipo ya kabla kufungwa, wateja kuhamishiana uniti za maji

0
80

Wizara ya Maji na Umwagiliaji inakusudia kuanza kufunga mita za maji za malipo ya kabla kwa ajili ya majaribio kati ya Julai na Spetemba mwaka huu ikiwa ni mkakati wa kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ambapp amesema kuwa mita hizo zitatua changamoto nyingi kwani mwananchi ataweza kununua maji akiwa sehemu yoyote, na mara tu atakaponunua yataanza kutoka bila kumlazimu yeye kufika kwenye mita na kuingiza tokeni.

Aidha, kama hiyo haitoshi amesema mita hizo zitamuwezesha mteja mmoja kumhamishia mteja mwingine uniti za maji, na akapata maji. Pia mtu anapohama kutoka nyumba moja kwenda nyinge ataweza kuhama na uniti zake zilizobaki.

“Ikitokea jirani yako ameishiwa maji na wewe katika hii mita ya pre-paid [malipo ya kabla] una maji, unaweza ukamgawia na akapata maji,” amesema Sanga.

Amewatoa hofu wananchi kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha tatizo la kimtandao halitokei na pia kunakuwa na njia mbadala endapo hitilafu ya kimtandao itatokea ambayo inaweza kuwafanya wananchi kushindwa kununua maji.

Mbali na faida zake nyingi, mita hizi zitaepusha pia wananchi kubambikiwa ankara za maji lakini pia usumbufu wa ulipaji wa ankara za maji, kwani mteja atatakiwa kulipia kwanza ndipo apate huduma.

Send this to a friend