Mjue Askofu Alex Gehaz Malasusa, Mkuu mpya wa KKKT

0
19

Mkutano Mkuu wa 21 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), umemchagua Askofu Alex Malasusa (62) kuwa Mkuu wa KKKT, akichukua nafasi kutoka kwa Askofu Dkt. Fredrick Shoo aliyemaliza muda wake.

Askofu Malasusa amerudi kushika wadhifa huo ambao aliutumikia kwa mara ya kwanza kuanzia mwaka 2007 hadi 2016.

Amechaguliwa kwa kura 167 sawa na asilimia 69.3 za kura zote 241 zilizopigwa huku Askofu Abednego Kesho Mshahara akipata kura 73 sawa na asilimia 30.3

Huu ni wasifu mfupi wa Askofu Alex Malasusa;

Alizaliwa Aprili 18, 1961 katika kijiji cha Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya. Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto nane ya Mchungaji Gehaz Japhet Malasusa na Mama Subilaga Timoth Malasusa.

Alisoma katika shule mbalimbali za msingi kutokana na kuhama kwa wazazi wake. Mwaka 1976 alihitimu shule ya msingi Bungo Morogoro na baadaye kujiunga na masomo ya sekondari katika shule ya Kigurunyembe mwaka 1977. Baada ya masomo ya sekondari alijiunga na Chuo cha Uongozi wa Biashara na baadaye alijiunga na masomo ya uhasibu.

Malasusa alifanya kazi katika mashirika mbalimbali likiwemo Shirika la Akiba la Taifa kwa miaka minne, na baadaye alijiunga na masomo ya Theolojia. Katikati ya masomo hayo, alipata fursa ya kusoma vyuo vingine vya nje katika mpango wa kubadilishana wanafunzi.

Alihitimu masomo mwaka 1995 na kubarikiwa kuwa Mchungaji katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani Septemba 03, 1995. Masomo na mafunzo mengine ni pamoja na Usimamizi na Utawala pamoja na mafunzo ya dini mbalimbali.

Mwaka 1996 alifunga ndoa na Ericah Simon Nkonoki na kubarikiwa watoto watatu, Miriam, Michael na Mercy.

Askofu Alex Malasusa amefanya kazi Chuo Kikuu (DSM), Usharika wa Mburahati, Usharika wa Yombo, Usharika wa Msasani na kuwa Mkuu wa Jimbo la Kinondoni (sasa Kaskazini). Pia Askofu amewahi kuwa Msimamizi wa Kiroho (Chaplain) wa Seminari ndogo Kisarawe.

Aidha, nyadhifa nyingine alizotumikia ni kuwa Mkuu wa KKKT kwa miaka 8 kuanzia mwaka 2007 hadi 2016 na Mkuu wa Chuo Kikuu Tumaini Makumira kwa kipindi chote.

Pia, amekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2017, na sasa ni Mwenyekiti wa CCT – Dar- es- Salaam.

Amekuwa Makamu wa Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani. (LWF) kwa miaka 7 tangu mwaka 2012 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu WCC. Amekuwa Mwenyekiti wa PROCUMURA Tanzania kwa miaka sita.

Malasusa amekuwa pia Mwenyekiti wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii Tanzania (CSSC) kwa miaka minne na kwa sasa ni Mwenyekiti wa CSSC kanda ya Mashariki na ni Mwenyekiti wa bodi mbalimbali ndani na nje ya kanisa.

Baadhi ya Vyuo Vikuu duniani vilivyomtunuku Shahada za Uzamivu za Heshima za Udaktari ni Trinity Lutheran University, Finlandia University vya Marekani na Helsink University cha Finland.

Send this to a friend