
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika (UNOAU), Parfait Onanga Anyanga, ambaye ni Mjumbe Maalum wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu UN ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua ilizochukua kurejesha amani na utulivu kufuatia vurugu na matukio ya uvunjifu wa amani zilizotokea Oktoba 29, 2025.
Onanga-Anyanga ametoa pongezi hizo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya mwanzo ya mazungumzo yake na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kitaifa.
Mjumbe huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi kwa lengo la kufanya mashauriano na Serikali na wadau wengine wa kitaifa kuhusu hali ya kisiasa nchini, pamoja na kujadili namna Umoja wa Mataifa unavyoweza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia maridhiano jumuishi.
Aidha, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha utulivu na uongozi makini katika kipindi hicho kigumu kwa taifa. Amekaribisha pia uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.








