Mkandarasi apiga TZS bilioni 64 mradi wa Bandari ya Tanga

0
59

Mbunge wa Viti Maalum, Judith Kapinga amesema mkandarasi mkuu aliyepewa tenda ya kufanya maboresho katika Bandari ya Tanga kwa kiasi cha Shilingi bilioni 104 alizopewa kutoka Serikalini aliigawa kazi hiyo kwa mkandarasi mwingine kwa kiasi cha shilingi bilioni 40 pekee.

Akifafua hayo leo bungeni Dodoma wakati wa kujadili taarifa za kamati zilizotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwaka 2020/21, amesema kampuni hiyo inayotambulika kwa jina la CHEC iliingia mkataba wa mwaka mmoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania Agosti 3, 2019 hadi Agosti 3, 2020 kwa ajili ya kazi kubwa tatu ambazo ni kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli, kufanya tathmini ya athari ya kimazingira na kununua vifaa kwa ajili ya shughuli za bandari.

Ameongeza kuwa kazi iliyotakiwa kufanyika ilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 176.36 huku kazi aliyompa mkandarasi mbia ilikuwa ni kuongeza kina na ujenzi wa gati ambayo iligharimu asilimia 60 ya fedha yote, na licha ya kuwa mkandarasi huyo kutakiwa kupokea shilingi bilioni 104 badala yake alipewa fedha pungufu ambazo ni shilingi bilioni 40.

Aidha, Kapinga amehoji kwanini jambo hilo halikuwekwa katika ripoti ya kamati wakati wa majumuisho yao ikiwa ni jambo ambalo linagusa maslahi ya Watanzania na fedha za umma, huku akidai viongozi wa mamlaka husika kuukalia kimya ubadhirifu huo.

Mbunge huyo ameliomba Bunge kuazimia hatua za haraka zichukuliwe kwa wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

Send this to a friend