Mke asimulia mume wake alivyofia kituo cha polisi

0
16

Uliriki Sabas (47) mkazi wa Kijiji cha Kirongo chini wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro amedaiwa kufariki akiwa mikononi mwa Polisi katika kituo cha Polisi cha Usseri wilayani humo baada ya kukamatwa akituhumiwa kujamiiana na mwanafunzi.

Akisimulia tukio hilo, Prisila Kavishe (42) ambaye ni mke wa marehemu amedai Septemba 7 mwaka huu mumewe alikamatwa na kufikishwa kituoni hapo, Septemba 6 alimpelekea mumewe chai na kumkuta akiwa mzima wa afya na kutaarifiwa kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani, hivyo ndugu wakatakiwa kuondoka kituoni hapo.

Ameongeza kuwa baada ya kufika nyumbani alipigiwa simu na jirani yake kuwa anatakiwa kituoni kuna tatizo. Alipofika kituoni alimkuta mumewe akiwa amelazwa sakafuni, huku akiwa na uvimbe mkubwa kichwani, majeraha mdomoni, jicho moja likiwa limeumizwa huku akivuja damu.

Akisimulia zaidi amesema, “niliuliza mume wangu amepatwa na nini? Askari wakasema wakati wanataka kumpeleka Ibukoni alitaka kuruka kwenye gari, na kwamba walipofika njiani wakawa wamemrudisha kituoni na kumweka mahabusu.”

“Wakaniambia walipomweka mahabusu alijigonga ukutani, askari wale wakawa wananiharakisha mchukueni mtu wenu mpelekeni kituo cha afya Karume,” ameongeza Prisila.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simoni Maigwa amesema tayari limefunguliwa jalada la uchunguzi wa kifo cha mtu huyo, na kwamba madaktari ndio watakaothibitisha kuwa amefariki kwa sababu gani.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend