Mkemia mkuu wa serikali athibitisha gongo ya mabibo kuwa salama

0
70

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa kutoa kibali kwa wakazi wa mkoa huo kuzalisha pombe za kienyeji kwa kutumia mabibo ya korosho, baada ya watalamu kueleza kuwa pombe hiyo haina madhara yoyote kwa binadamu.

Gelasius Byakanwa ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha majibu ya sampuli ya pombe ya mabibo (gongo) iliyopelekwa katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kujua usalama wa kinywaji hicho, ikiwa ni hatua inayolenga kukuza viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa za ndani.

“…ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema kuwa vileo hivyo [vinavyotumika kutengeneza gongo ya mabibo] ni salama na havina sumu aina yoyote. Nimemuandikia barua waziri wa viwanda na biashara kumtaka kutumia mamlaka aliyonayo kutangaza mabibo kuwa zao halali la kutumika kuzalisha pombe za kienyeji au gongo,” amesema Byakanwa akizungumza na waandishi wa habari.

Mbali na kuwataka wazalishaji wa pombe hiyo kujisajili ili waweze kutambulika pamoja na uwezo wao wa kuzalisha, ameliagiza jeshi la polisi kuacha mara moja kuwakamata wazalishaji wote watakaokuwa wamesajiliwa.

“‘Kwa kuwa tumepiga gongo hiyo na kukuta ni salama, na kwa kuwa tumeomba kibali cha waziri cha kuzalisha, nilitake jeshi la polisi kuacha kuwakamata wale wote watakaokuwa wamejisajili kwenye halmashauri zetu,” amehitimisha Byakanwa.

Send this to a friend