Mkenda: Walimu wakuu waliovuliwa vyeo kama wameonewa wakate rufaa

0
48

Baada ya Serikali kuwavua vyeo wakuu wawili wa shule kwa kuruhusu wimbo wa mwanamuziki Zuchu ‘Honey’ kupigwa shuleni bila ya wao kuchukua hatua, Waziri wa Elimu, Prof. Adolph Mkenda amesema endapo adhabu hiyo haikuwatendea haki ikiwemo kutokuwepo shuleni siku ya tukio, basi walimu hao wakate rufaa.

Akizungumza bungeni leo wakati akijibu swali la Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson alilohoji ikiwa walimu hao walikuwepo shuleni au la, amesema “hilo ni suala la kinidhamu kama walikuwa hawapo wanaweza kukata rufaa kwa mkurugenzi ambaye ndiye amewaondoa katika mamlaka.

Kama mtu amechukuliwa hatua kinyume na taratibu kwa mfano hakuhusika moja kwa moja kuna fursa ya kukata rufaa, sisi tulitoa wito kwa mkurugenzi ambaye ndiyo mamlaka yake ya nidhamu.”

Wakuu wa shule wavuliwa nyadhifa zao kisa wimbo wa Zuchu (Honey)

Aidha, Dkt. Tulia ametoa wito kwa waziri kwamba, kama walimu hao hawakuwepo shuleni na mamlaka ya nidhamu imechukua hatua kabla ya kufanya uchunguzi, basi walimu hao warejeshwe kwenye nafasi zao.

Hata hivyo, Prof. Mkenda ametoa wito kwa walimu wakuu kusimamia maadili shuleni na kudhibiti miziki inayokiuka maadili ya Kitanzania kama vile kupiga miziki inayochochea ngono, pombe, sigara na kadhalika ikiwemo kwenye mabasi ya shule huku akisisitiza kuwa si kila kitu kinachokubaliwa uraini kinakubaliwa shuleni.

Send this to a friend