Mkenya aajiriwa kwenye nafasi za juu za mashirika 8 ya umma

0
41

Kaimu Katibu na Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Elimu ya Kisheria (CLE), Jennifer Gitiri, anakabiliwa na tuhuma za kushikilia nafasi kadhaa katika ofisi za umma hivyo kuwanyima haki Wakenya wengine wanaostahili kuhudumu katika nafasi hizo.

Katika ombi lililowasilishwa katika Mahakama Kuu, Dkt. Magare Gikenyi amesema Gitiri amekuwa akichota mishahara na marupurupu kutoka kwa hazina ya kitaifa kwa kushikilia nyadhifa nane za umma, hatua aliyotaja kuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka ya utawala.

Dkt. Gikenyi alidokeza kuwa Gitiri ndiye Naibu Mkurugenzi wa Wakala wa Urejeshaji Mali (ARA), katibu wa shirika hilo, kaimu afisa mkuu mtendaji na kaimu katibu wa CLE, na pia anahudumu kwenye bodi kadhaa kama Mwanasheria Mkuu.

Ameitaka mahakama itoe amri ya kumkataza kuhudumu kama mwanachama wa Bodi au mfanyakazi wa Baraza la Elimu ya Sheria, Baraza la Kuripoti Sheria la Kenya (KLRC), Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA), wakala wa Ulinzi wa mashahidi (WPA) na wakala wa Ulinzi wa Waathiriwa (VPA).

“Ningependa kusema kwamba Gitiri hana ujuzi mkubwa unaomfanya kuwa na sifa bora zaidi kuliko mawakili wa Serikali 800 wanaofanya kazi katika mabaraza ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao wanaweza na vile vile wanapaswa kuteuliwa katika bodi za umma kama mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” ameeleza katika nyaraka za mahakama.

Send this to a friend