Mkenya aliyehukumiwa kifo Vietnam apunguziwa adhabu

Raia wa Kenya, Margaret Nduta Macharia (37) ameepukana na adhabu ya kifo baada ya Mahakama Kuu ya Vietnam kubadili hukumu yake ya kifo na kuwa kifungo cha maisha jela, kufuatia shinikizo la kidiplomasia na kampeni ya haki za binadamu kutoka ndani na nje ya Kenya.
Margaret alihukumiwa kifo Machi mwaka huu baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha zaidi ya kilo mbili za kokeini kuingia nchini Vietnam, ambapo sheria za dawa za kulevya ni kali na adhabu ya aina hiyo ni kifo kwa njia ya sindano ya sumu.
Viongozi wa Kenya walijitokeza kushinikiza kuokolewa kwa maisha ya Margaret. Juhudi zao ziliungwa mkono na mashirika kadhaa ya kiraia yaliyodai kuwa Margaret huenda alikuwa mhanga wa usafirishaji haramu wa binadamu, aliyetumiwa katika biashara hiyo ya dawa ya kulevya na sio matakwa yake.
Watetezi wa haki za binadamu walikosoa hukumu ya awali kwa kusema kuwa kunyonga watu kama Margaret hakutamaliza biashara ya dawa za kulevya bali kunawaadhibu walioko katika mazingira magumu wakiitaka Vietnam kuonesha huruma na kuheshimu misingi ya haki na utu.








