Mkurugenzi apendekeza bodaboda kutoingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam

0
58

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri amesema kuwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam lipo katika harakati za kujenga vituo maalum 15 kwa ajili ya waendesha pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda.

Akizungumza na gazeti la Nipashe, amebainisha kuwa vituo hivyo vitajengwa kwenye barabara zinazoingia katikati ya jiji hilo na kwa sasa bado hawajakubaliana na watu wa bodaboda kuhusu maeneo gani hasa ya kujenga vituo hivyo.

“Bodaboda walikuwa wanataka waingie mpaka katikati ya jiji na tulisema wasiingie katikati, tunapanga mji kwa ushirikiano na wenye bodaboda, hivyo vitakuwepo vituo 15 ambavyo tumeviainisha na kuhusu maeneo bado tunaendelea kuzungumza nao, vituo vikikamilika tutawaambia,” amesema mkurugenzi.

Aidha, aliongeza kuwa itapendeza zaidi kama bodaboda hawatoingia katikati ya mji na badala yake washushe abiria katika maeneo maalum yatakayotengwa.

“Tulifikiria mfano maeneo ya Kamata au kama unaingia mjini kwa kutokea Magomeni boda boda wanabaki eneo la Fire, hapo ndipo wanachukua watu kutoka katikati ya jiji kuwapeleka nje ya jiji,” ameongeza.

Send this to a friend