Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri na watumishi wengine tisa kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa TZS bilioni 10 za Serikali ambazo zilikusanywa na hazikuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.
Agizo hilo linatokana na matokeo ya ukaguzi maalumu kuhusu mapato ya ndani katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2020/2021 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Majaliwa ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, wabunge, madiwani pamoja na watumishi wa wilaya ya Ilala katika ukumbi wa Karimjee akiwa katika ziara yake ya kikazi Dar es Salaam.
“Watumishi hao wanatuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kuisababishia halmashauri hasara ya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 10 zilizokusanywa na mawakala na watumishi wa Halmashauri hiyo lakini hazikuingizwa benki” amesema.
Aidha, watumishi hao pia wamekabidhiwa kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dar Es Salaam kwa mahojiano juu ya tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ufuatilie vyanzo vyote vya mapato vya halmashauri hiyo na pia waweke makadirio ambayo yatawawezesha kukusanya zaidi.
Pia amewasisitiza waweke makadirio yatakayowawezesha kufanya kazi zaidi na kila muhusika ahakikishe anatekeleza majukumu yake ipasavyo.