Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) , Ernest Khisombi amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili kwa tuhuma za kujipatia mkopo wa gari binafsi wenye thamani ya TZS milioni 196 kinyume na sheria ya maadili ya viongozi wa umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Akisoma mashtaka mbele ya Baraza la Maadili, Wakili wa Serikali, Hassan Mayunga ameliambia baraza kuwa, mtuhumiwa anashtakiwa kwa makosa mawili ambayo ni kukopa fedha za mfuko kiasi cha TZS milioni 117.9 bila kufuata utaratibu pamoja na kulipiwa kodi kiasi cha TZS milioni 78.8 bila kufuata utaratibu wa sera ya mikopo ya PSSSF.
Kwa mujibu wa Mayunga, kitendo hicho kinamfanya Khisombi ambaye ni kiongozi wa umma kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma kushidwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) na (b) na hivyo kukiuka maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Hata hivyo, Khisombi amekana tuhuma hizo na kulieleza Baraza la Maadili kuwa, “fedha hizi ni haki yangu kama Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi kwa mujibu wa Sera ya Mikopo ya Mfuko.”