Mkurugenzi wa Wilaya anunua dawa ya mchwa kwa TZS 66 milioni

0
31

Rais Dk John Pombe Magufuli leo Agosti 1 ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kayombe Liyoba kutokana na usimamizi usioridhisha wa miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.

Akitoa taarifa hiyo leo Waziri wa TAMISEMI, Sulemani Jafo amesema kuwa mkurugenzi huyo ameshindwa kusimamia fedha za serikali na pia amekiuka sheria za manunuzi ya umma.

Waziri Jafo amesema kuwa katika ujenzi wa hospitali hiyo, mkurugenzi alinunua dawa ya kupilizia mchwa kwa TZS 66 milioni, kiasi ambacho ni zaidi ya matumizi yaliyokuwa yanatarajiwa.

Aidha mkurugenzi huyo ameshindwa kufuata taratibu za ujenzi wa hospitali hiyo na sheria za manunuzi ya umma kwani imebainika kuwa kokoto zilinunuliwa kwa zaidi ya TZS 45 milioni na zilisafirishwa kwa TZS 42 milioni.

Kufuatia mapungufu hayo, Rais ametengua uteuzi huo na nafasi hiyo itakaimiwa na Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wa Wilaya ya Morogoro Vijijini, Mhandisi Godfrey Mlowe.

Waziri Jafo amemuagiza meneja huyo kuhakikisha ujenzi wa hospitali ya wilaya unakamilika, na hali kadhalika ujenzi wa vituo viwili vya afya vya Mikese na Kinonko vilivyopelekewa fedha hivi karibuni.

Send this to a friend