Mlipuko wa virusi vya Nipah India waibua hofu Asia

0
31

Baadhi ya nchi za Asia zimeanza kuchukua hatua za ukaguzi kwa wasafiri katika viwanja vya ndege na mipakani kufuatia mlipuko wa virusi vya Nipah katika Jimbo la West Bengal, nchini India.

Nchini Thailand, mamlaka zimeanza kuwafanyia ukaguzi wa kiafya abiria katika viwanja vitatu vya ndege vinavyopokea safari kutoka West Bengal, huku Nepal ikianza ukaguzi wa wasafiri wanaoingia kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kathmandu pamoja na vituo vya mipaka ya nchi kavu vinavyounganisha taifa hilo na India.

Taarifa za Wizara ya Afya ya India zinaeleza kuwa visa viwili vya virusi vya Nipah vimethibitishwa tangu Desemba, vikihusisha wahudumu wa afya. Aidha, watu 196 waliokutana na wagonjwa hao wamefuatiliwa na kupimwa, na wote wamekutwa hawajaambukizwa.

Virusi vya Nipah huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, hususan popo- matunda na nguruwe, na pia vinaweza kusambaa kutoka mtu kwenda mtu kupitia majimaji ya mwili. Hakuna chanjo wala dawa maalum.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, dalili za Nipah hujitokeza ndani ya siku 4 hadi 14 baada ya maambukizi. Dalili za awali ni pamoja na homa, maumivu ya Kichwa, maumivu ya misuli, kutapika na maumivu ya koo.

Aidha, kwa baadhi ya wagonjwa dalili zinaweza kuongezeka na kusababisha kusinzia kupita kiasi, kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu na nimonia.

Send this to a friend