Mmoja wa mapacha waliotenganishwa afariki

0
72

Neema, mmoja wa mapacha waliotenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Julai 1, 2022 amefariki dunia.

Muhimbili imeeleza kuwa Neema na Rehema walifanikiwa kuvuka saa 72 ambazo ni hatarishi, lakini bado walikuwa chini ya uangalizi maalum (ICU), lakini hali ya Neema ilibadilika ghafla Jumapili asubuhi.

“[Neema] akiwa ICU hali yake ilibadilika ghafla, madaktari walijitahidi kurudisha hali yake bila mafanikio na hatimaye kupoteza maisha, tuendelee kumwombea Rehema ambaye bado yupo ICU ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, Bwana alitoa na Bwana ametoa, jina lake lihimidiwe sana,” muhimbili imeeleza.

Upasuaji wa kuwatenganisha pacha waliokuwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo (Neema na Rehema) wenye umri wa miezi tisa ulifanyika kwa mafanikio katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo jopo la wataalamu 31 walitumia saa saba kukamilisha upasuaji huo.

Tanzania imekuwa nchi ya tatu barani Afrika kufanya upasuaji wa aina hii baada ya Afrika ya Kusini na Misri.

Send this to a friend