Mo Dewji: Siwekezi Simba ili nipate faida

0
49


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, Mohammed Dewji amesema kuwa uwekezaji anaofanya katika klabu hiyo si ili apate faida, bali ni kutokana na kuipenda Simba.

Mo Dewji amesema hilo mapema leo asubuhi akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, mkutano ambao ameutumia kueleza kuhusu maendeleo ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu.

Ameeleza kuwa, kikubwa katika uwekezaji wa Simba si fedha, bali ni muda, na kwamba anatumia muda mwingi kuisaidia Simba hadi wakati mwingine anapoteza fursa za kufanya biashara zake nyingine.

Aidha, ametumia mkutano huo kukabidhi hundi ya TZS bilioni 20 kwa Simba SC ikiwa ni fedha za hisa asilimia 49 alizonunua baada kubadilishwa kwa mfumo wa uendeshaji kutoka timu ya wanachama pekee, na kuruhusu wanachama na mwekezaji.

“Leo naweka hiyo bilioni 20 ya hisa asilimia 49 mbele ya mdhamini wa klabu na mwenyekiti wa klabu,” amesema MO.

Pia amedokeza kuwa katika miaka minne iliyopita ametumia TZS bilioni 21.3 ndani ya klabu hiyo, fedha zilizotumika katika usajili, mishahara, maandalizi ya misimu na shughuli nyingine, na bado anatendeleankuwekezs kuifanya Simba kuwa imara.

Kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji amesema tayari Tume ya Ushindani (FCC) imeidhinisha mabadiliko hayo na wameruhusiwa kukamilisha mchakato.

Dewji ambaye alikuwa ameambatana na Mwenyekiti wa Simba na mdhamini mkuu, amesema kuwa klabu hiyo imebadilisha hadhi ya soka la Tanzania, na kwamba sasa lengo lao ni kutwaa ubingwa wa Afrika.

Amewaonya viongozi na wanachama kutambua kuwa hakuna mtu yeyote (hata yeye mwenyewe) aliye mkubwa kuliko Simba.

Send this to a friend