Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Profesa Abel Makubi amesema asilimia 60 ya majeruhi wa ajali hasa ajali zinazohusiana na bodaboda wanaumia sehemu za ubongo.
Ameyasema hayo katika mkutano wa kimataifa wa Wataalam wa Ubongo, mishipa ya fahamu na uti wa mgongo uliondaliwa na MOI kwa kushirikiana na Chuo na Hospitali ya Well Cornel ya nchini Marekani.
“Kwa wastani kwenye idara ya magonjwa ya dharura, tunapokea wagonjwa 15 hadi 20 ambao wanatokana na dharura mbalimbali na asilimia 60 zinatokana na ajali na wengi ni bodaboda. Tatizo ni kubwa wengi wanakuwa wameumia mifupa na ubongo,” ameeleza.
Amesema mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam wa siku nne unaotoa mafunzo ya tiba yanayotokana na ajali zinazoumiza ubongo, yatawasaidia wataalamu kuwatibu wananchi walioumia kwa ajali zilizoathiri ubongo na mgongo.