Mfalme wa Morocco, Mohammed VI ametoa msamaha kwa takriban watu 5,000 waliokuwa wamehukumiwa au wanaosakwa kwa makosa yanayohusiana na kilimo cha bangi haramu.
Taarifa kutoka Wizara ya Sheria ya nchi hiyo imesema kuwa msamaha huo utawatia moyo wakulima kushiriki katika mchakato wa kisheria wa kulima bangi ili kuboresha mapato yao na hali ya maisha.
Morocco, ambayo ni moja ya wazalishaji wakubwa wa bangi duniani, iliidhinisha sheria mwaka 2021 inayoruhusu kilimo, usafirishaji na matumizi ya bangi kwa madhumuni ya matibabu na viwanda, lakini matumizi ya bangi kwa starehe bado hayaruhusiwi.
Kwa mujibu wa Mohammed El Guerrouj, mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bangi ya Morocco (ANRAC), uzalishaji wa bangi halali ulifikia tani 294 za metriki mwaka 2023, huku takriban kilo 225 zikiwa zimesafirishwa nje ya nchi tangu mwaka huo.
Uzalishaji wa mwaka huu unatarajiwa kuongezeka kutokana na idadi ya vibali vya kilimo kuongezeka na ANRAC kuruhusu kilimo cha aina ya bangi ya kiasili inayojulikana kama Beldia.