Morrison asimamishwa Yanga kwa utovu wa nidhamu

0
57

Mchezaji wa Klabu ya Yanga, Benard Morrison anadaiwa kusimamishwa na Kocha wa klabu hiyo, Nasreddine Nabi kutokana na utovu wa nidhamu.

Taarifa zinadai kuwa mchezaji huyo alipewa adhabu hiyo na wachezaji wengine wawili wa klabu hiyo, Djuma Shaban na Farid Mussa ambao kwa ujumla wamekosekana kwenye mechi tatu za Ligi Kuu Bara, kutokana na utovu wa nidhamu.

Inadaiwa kuwa wachezaji hao waliondolewa kikosini kutokana na kuchelewa kuripoti kambini baada ya kupewa mapumziko ya siku mbili kwa kikosi cha Yanga baada ya kumaliza mechi ya ligi dhidi ya Kagera Sugar na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Wakati Farid na Djuma wakirejea kwenye kikosi hicho, inasemekana kuwa Morrison amepelekwa kwenye kamati ya maadili ya klabu hiyo kwa ajili ya utovu wa nidhamu.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kimeiambia Mwanaspoti, wachezaji hao walishindwa kuripoti kambini siku iliyokuwa imepangwa na siku iliyofuatia waliporudi Kocha Nabi akawatimua.

“Wachezaji hao walizingua na kocha Nabi akawapa adhabu ya kimya kimya, ila tayari wameshaomba radhi na kurejeshwa kikosi na wameingia kambini na wenzao tayari kwa mchezo ujao dhidi ya Prisons,” kimesema chanzo hicho kutoka ndani ya Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti

Send this to a friend