Mpangaji auza nyumba ya mwenye nyumba na kutoweka na pesa

Kesi ya kushangaza ya ulaghai imeibuka nchini Nigeria baada ya mpangaji kudaiwa kuuza nyumba ya mwenye nyumba wake yenye vyumba vinne kwa thamani ya ₦83 milioni [TZS milioni 136.2] kisha kutoweka na fedha hizo.
Kwa mujibu wa wakili mmoja wa Nigeria anayejulikana TikTok kama @theomonilelawyer, mpangaji huyo aliishi katika nyumba hiyo kwa zaidi ya miaka saba kabla ya kutekeleza njama hiyo. Inadaiwa alighushi nyaraka muhimu kama hati ya uhamisho, ramani ya ardhi na risiti zinazodaiwa kutolewa na familia ya Okota, kisha akamshawishi mnunuzi kuamini mali hiyo ilikuwa halali na inauzwa.
Baada ya kupokea malipo yote, mpangaji huyo alidai anahitaji muda wa miezi minne zaidi ili kuhama, akitumia kisingizio cha kutafuta makazi mapya. Hata hivyo, baadaye ilibainika kupitia wakala kuwa mtu huyo, aliyedhaniwa kuwa mpangaji, alijitambulisha kwa mnunuzi kama mmiliki halali wa nyumba hiyo.
Mwenye nyumba, ambaye amerudi Nigeria hivi karibuni, ameripoti tukio hilo kwa polisi na uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika.
Wakili huyo aliyetangaza kesi hiyo amewatahadharisha wananchi kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kununua nyumba au ardhi, akisisitiza: “Hakikisha kwanza kabla hujanunua. Usije ukaingia mtego wa matapeli wa mali.”








