Mpina akabidhiwa kwenye Kamati ya Maadili juu ya ushahidi wa Bashe kwa vyombo vya habari

0
44

Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ameiagiza Kamati ya Haki Maadili na Madaraka ya Bunge kukutana na kujadili juu ya mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kuwasilisha kwa vyombo vya habari nyaraka za ushahidi aliomtuhumu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kusema uongo bungeni kabla ya taarifa hizo kuwekwa mezani na kujadiliwa na bunge.

Akitoa taarifa hiyo bungeni, Spika Tulia pia ameielekeza kamati hiyo ipitie ushahidi wa mbunge huyo na kutoa maoni iwapo ushahidi huo unathibitisha tuhuma za kuwa Waziri Bashe amesema uongo bungeni.

“Mheshimiwa Mpina amekuwa bungeni kuanzia mwaka 2005 hivyo ni mbunge mzoefu na anazifahamu ipasavyo sheria, kanuni na taratibu zinazoliongoza bunge. Ni dhahiri kitendo cha yeye kuwasilisha nyaraka za ushahidi kwangu na kwenye vyombo vya habari kuhusu mahudhui ya nyaraka hizo ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa bunge na spika, kudharau mamlaka ya spika, kuingilia mwenendo wa bunge na kushusha hadhi na heshima ya bunge,” amesema.

Hoja iliyosababisha Mpina kutakiwa kuwasilisha uthibitisho kwa Spika Juni 14, 2024 inahusu kiwango cha uagizaji wa sukari ya ziada nje ya nchi katika kipindi ambacho viwanda vinakuwa vimesimamisha uzalishaji, ambapo Mpina alidai kuwa kwa mujibu wa sheria uagizaji wa sukari nje ya nchi kwa ajili ya kuziba pengo unatakiwa uwe takriban tani 150, 000 na zabuni itangazwe.

Hata hivyo, Mpina amedai Wizara ya Kilimo haikutangaza zabuni na imetoa vibali kwa wasioruhusiwa na sheria kupata kibali cha kuagiza sukari nje, ikiwamo kuagiza tani nyingi zaidi ya tani laki nne.

Akijibu hoja hizo, Waziri Bashe alisema kuwa hakuna zabuni kwa uagizaji wa sukari ya kuziba pengo kutokana na viwanda vya ndani kusimamisha uzalishaji kwa miezi mitatu ya msimu wa mvua.

Pia, Bashe alisema walitoa vibali kwa viwanda vya ndani kuagiza sukari, lakini hakuna kiwanda kilichoingiza hata kilo moja ya sukari na kusababia kilo moja ya sukari kuuzwa hadi shilingi 10, 000.

Kwa mujibu wa Spika, Mpina anaweza kukabiliwa na adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao kumi mfululizo vya bunge.

Send this to a friend