
Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imewapendekeza wanachama wake Aaron Kalikawe na Luhaga Mpina kuwania kugombea nafasi ya urais wa Tanzania.
Kwa upande wa Zanzibar, chama hicho kimempendekeza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman akiwa mwanachama pekee aliyechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo majina ya wagombea yaliyopendekezwa yatawasilishwa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa ajili ya kupigiwa kura.
Kwa upande mwingine, chama hicho kimesema kimepokea na kuridhia hatua ya mgombea wake, Dorothy Semu kujitoa kugombea nafasi ya urais wa Tanzania.
Semu ambaye ni kiongozi wa chama hicho ameieleza Halmashauri Kuu kuwa amechukua hatua hiyo katika kutekeleza wajibu wake wa kiuongozi wa kukiwezesha chama kutekeleza wajibu wake wa kimapambano wa kukiondosha Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.







