Mradi bandari ya Kilwa kuzalisha ajira 20,000

0
22

Rais Samia Suluhu Hassan amesema fedha zinazotolewa na Serikali kwa wananchi ni kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na si kwa ajili ya kuwanufaisha viongozi.

Ameyasema hayo wilayani Kilwa mkoani Lindi Septemba 19, 2023 wakati wa uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa bandari ya uvuvi pamoja na kugawa boti za kisasa kwa wavuvi na wakulima wa mwani ambapo jumla ya boti 160 zimetolewa kwa mkopo wa masharti nafuu.

“Kwa mtiririko huu wa fedha zinavyokuja ndani ya wilaya yenu, Kilwa isipobadilika naomba mkae kitako mjitazame wenyewe kuna nini, lakini kwa serikali tunajitahidi kumimina fedha […] Hizi fedha zinaletwa kwa ajili ya kuondosha dhiki na changamoto za wananchi, hizi fedha haziletwi viongozi mjinufaishe,” amesema.

Zanzibar yakabidhi uendeshaji wa bandari kwa mwekezaji

Aidha, Rais Samia amesema kupitia mradi huo wa bandari ambao utachukua takribani jumla ya miezi 36 na kugharimu TZS bilioni 266, utafungua fursa mbalimbali katika sekta ya uvuvi na biashara kwa ujumla ambapo takribani ajira 20,000 zinatarajiwa kuzalishwa.

Mbali na hayo, amesema kutokana na meli nyingi za kimataifa ambazo zitaingia nchini, Serikali inapanga kujenga bandari nyingine ya uvuvi Bagamoyo ikiwa hali ya uchumi itaruhusu.