Msajili avionya vyama vya siasa kuhusu uchochezi na lugha za dhihaka

0
36

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amevionya vyama vya siasa kuepuka lugha za uchochezo, dhihaka, dharau na vitisho wakati vikiendelea kunadi sera zake kwa wananchi.

Aidha, Jaji Mutungi amevitaka vyama vyote kufanya siasa za kistaarabu, kuvumiliana na kuheshimu sheria za nchi.

“Demokrasia inatekelezeka vyema mahali ambapo watu wanaheshimu sheria za nchi, wanafanya siasa za kistaarabu,” ameeleza Mutungi kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Ameongeza kuwa vyama vya siasa vipo katika jamii ambayo ina watu ambao ni wanachama wa vyama mbalimbali na wengine hawana vyama, hivyo ni vyema vyama vya siasa vikafanya shughuli zake kwa kuzingatia maslahi na haki za watu wengine kwa ujumla wake.

Onyo la Jaji Mutungi limekuja siku tatu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka wananchi kupuuza wanaozua chokochoko kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi.

“Kuna baadhi ya watu wameshaanza chokochoko naomba muwapuuze kwani hawawatakii mema, wanataka kuvunja amani ya nchi iliyopo kwa muda mrefu na kusababisha vurugu nchini,” alisema Rais akiwa mkoani Morogoro.

Licha ya kuwa Rais na Msajili wa Vyama vya Siasa hawajaeleza ni watu gani hao, lakini kutokana na hali ya sasa unaweza kuhusianisha haya na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanarakati mitandaoni ambao wamekuwa wakishinikiza kupatikana kwa katiba mpya.

Watu hao wamekuwa wakimtaka Rais kuanzisha mchakato wa katiba mpya kwa maelezo kuwa katiba ya sasa ina mapungufu mengi.

Send this to a friend