
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebatilisha uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT Wazalendo, ikisema amekosa sifa za kuwa mgombea wa nafasi hiyo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia Katibu Mwenezi Mkoa wa Dar es Salaam wa chama hicho, Monalisa Ndala kuwasilisha malalamiko kwenye ofisi hiyo akieleza dosari za kikatiba na kikanuni katika mchakato wa uteuzio wa mgombea huyo, ambapo ofisi ya msajili iliwakutanisha pamoja na viongozi wa chama.
Barua iliyotolewa na Ofisi ya Msajili imekubaliana na hoja za Bi. Ndala kuwa kanuni za Uchaguzi za ACT Wazalendo za mwaka 2024 zinatumika pia katika kuteua wagombea wa nafasi za kiserikali ikiwemo Urais, kwa maana kuwa mgombea huyo amekosa sifa ya kutokuwa mwanachama kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza.
Pia barua hiyo imekubaliana kuwa mwisho wa kuchukua fomu za kuomba uteuzi ulikuwa Mei 25, 2025 kabla Mpina kuwa mwanachama, hivyo mgombea huyo yuko nje ya muda wa kimchakato wa kikanuni za kiuchaguzi.
“Kwa msingi huo, Msajili wa Vyama vya Siasa ametamka wazi kwamba uteuzi wa Luhaga Joelson Mpina ni batili kisheria na hivyo hastahili kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya ACT Wazalendo,” ameseeleza Bi. Ndala kwenye taarifa yake kwa umma.
Mpina alikuwa mwanachama wa ACT Wazalendo Agosti 5, 2025 siku moja kabla ya kutangazwa na Mkutano Mkuu wa chama Agosti 06, mwaka huu.






