Msamvu: Mpigadebe afariki baada ya kuchomwa kisu na mwenzake wakigombea abiria

0
48

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu amethibitisha kutokea kifo cha Tazani Mdeme, mkazi wa Mwembesongo na mpigadebe wa kampuni ya mabasi ya BM Coach.

Mdeme amefariki dunia baada ya kudaiwa kuchomwa kisu na Abdallah Yassin mkazi wa Kihonda, mpigadebe wa kampuni ya mabasi ya Abood wakati wakigombea abiria katika Stendi Kuu ya Mabasi Msamvu, Morogoro.

Akizungumza shuhuda wa tukio hilo Sadick Zingwe, ameeleza kuwa wapigadebe hao walikuwa wakigombea abiria, walianza kubishana ndani ya stendi eneo la kuegesha magari na baadaye wakaamua kutoka nje na kuanza kupigana huku wakisisitiza mtu yoyote kutoingilia kati.

“Baada ya kupigana kwa muda mrefu mmoja alizidiwa na kuamua kutoa kisu na kumchoma mwenzake kifuani upande wa kushoto. Alikamatwa muda huo huo na askari na baadaye tukapata taarifa kuwa amefarik,” amesema shuhuda.

Mtuhumiwa Abdallah amekamatwa na hatua za kumfikisha mahakamani zitafuata mara upelelezi utakapokamilika.

Hata hivyo Kiongozi na Msemaji wa Kampuni ya BM, Joseph Mosha amesema kuwa mtafaruku uliotokea umesababishwa na kukiukwa kwa mpangilio wa namna ya upakiaji wa magari ndani ya stendi, kwani baadhi ya mabasi huegeshwa eneo lisilo rasmi na kwamba wamekuwa wakitoa taarifa kwa wahusika.

Send this to a friend