MSD ilivyofuja mamilioni ya UVIKO19 katika manunuzi ya vifaa

0
11

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya maafisa ununuzi wa umma kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko na kuahidi kuwa ataanza na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) kulishughulikia suala hilo.

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo wakati akizungumza na wataalamu wa ununuzi na ugavi pamoja na wasimamizi kwenye uzinduzi wa Wiki ya Ununuzi wa Umma jijiji Arusha.

“Pamoja na uwepo wa taasisi zinazosimamia manunuzi yanayofanywa katika ofisi zetu, bado wasimamizi wa manunuzi hawajaona huruma kwa walipakodi wetu kwa kuendelea kufanya manunuzi kwa gharama kubwa,” amesema.

Amesema kupitia fedha ya UVIKO-19 ambayo Rais Samia Suluhu Hassan alienda kukopa nje, ilitolewa fedha kupitia Wizara ya Afya ili zinununue vifaa vya tiba kwa ajili ya hospitali za mikoa, za rufaa, vituo vya afya na zahanati kwa nia ya kuwapunguzia mzigo Watanzania wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za tiba.

“MSD ilipata mgao wa fedha na ilipaswa kununua baadhi ya vifaa na nataka nitoe mfano huu; Walipaswa kununua kipimo cha sukari (blood glucose test) kwa TZS 150 lakini wao walikinunua kwa TZS 300. Walipaswa kununua kifaa cha kupima mkojo (urinalysis) kwa TZS 200 lakini wao walikinunua kwa TZS 780.”

Amesema walitakiwa kununua kipimo kidogo cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa TZS 2,100 lakini wao walikinunua kwa TZS 4,500; pia walitakiwa kununua kipimo kikubwa cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa TZS 3,800 lakini wao walikinunua kwa TZS 6,300; na walitakiwa kununua kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa figo na ini (Renal and Liver Function Test) kwa TZS 6,000 lakini wao walikinunua kwa YZS 40,000.

Akitoa mfano mwingine, Waziri Mkuu amesema MSD walipaswa kununua mashine ndogo ya kupimia kemia ya mwili (chemistry analyzer-semi automated) kwa TZS milioni 1.3 lakini wao waliinunua kwa TZS milioni 6.7, ilhali mashine kubwa ya kupimia kemia ya mwili (chemistry analyzer-full automated) iliyopaswa kununuliwa kwa TZS milioni 10.5 wao waliinunua kwa TZS milioni 49.

“Walipaswa kununua mashine kubwa ya kupimia hematolojia ya mwili (hematology analyzer 5-part dff full automated) kwa TZS milioni 20.8 lakini wao waliinunua kwa TZS milioni 117. Walipaswa kununua mashine ya kupima mfumokinga wa mwili (Immunology Analyzer Full Automated) kwa TZS milioni 37.4 lakini wao waliinua kwa TZS milioni 149.7,  na pia mashine ya kuchata maji kwa ajili ya kutumika katika kusafisha damu walipaswa kuinunua kwa TZS milioni 32.6 lakini wao waliinunua kwa TZS 129.”

“Niambieni ni kweli aliyepokea fedha hizo bado anazo? Je! Huyu aliyeendesha hilo zoezi hajaenda kufuata fedha nyingine?” amehoji.

Amesema Jumatatu atakwenda ofisi za MSD na hatosita kwenda na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni.

Send this to a friend