Msitishwe na Corona, chapeni kazi: Rais Dkt Magufuli

0
45

Rais Dkt Magufuli amewataka Watanzania kutotishwa na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchapa kazi na kujenga uchumi huku wakizingatia tahadhari zote za kujikinga kuambukizwa ugonjwa huo kama zilivyotolewa na wataalamu.

Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Machi, 2020 alipohudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Onesmo Wisi.

“Watu tusitishane, tunatishana mno. Niwaombe ndugu Wakristo na Watanzania kwa ujumla wa Madhehebu yote, huu ndio wakati mzuri sana wa kumtegemea Mungu kuliko wakati wote, tuendelee kuchapa kazi, tuendelee kuujenga uchumi wetu, hatuwezi kusalimu amri kwa ugonjwa huu wa Corona na kushindwa kumtegemea Mungu na tukashindwa kuendeleza uchumi wetu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amekemea tabia za baadhi ya watu wanaofanya mzaha juu ya ugonjwa huu ama kuwatia hofu wananchi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Aidha, amewashukuru viongozi wa Dini kwa kuungana na Serikali katika kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari na ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aepushe balaa hili la Corona.

Send this to a friend