Mtaalamu: Hakuna majibu ya Malaria 1, 2 au 3, wataalamu wanakiuka

0
50

Ofisa Mteknolojia wa Maabara kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Peter Torokaa amesema hakuna majibu ya maabara yanayoonesha mgonjwa kuwa na malaria 1,2 au 3 kama ambavyo wagonjwa wengi huambiwa.

Akizungumza wakati akiendesha mafunzo ya afya jijini Dar es Salaam, amefafanua kuwa baadhi ya wataalamu wa maabara wa vituo vya kutolea huduma za afya wamekuwa wakipotosha kwenye uchunguzi wa malaria na hivyo kutoa majibu yasiyokuwa sahihi.

Torokaa ameeleza kuwa kwenye tone moja la damu kuna uwezekano wa kuwa na seli nyeupe za damu zaidi ya 5000, hivyo mtaalamu wa maabara anapaswa kuanza kuhesabu seli nyeupe za damu pindi anapoona kimelea wa malaria. Hivyo Kuna uwezekano wa kuuona vimelea 1000 kwenye kila seli 1 nyeupe ya damu.

Mashirika 19 ya umma yaunganishwa na kubakia 7

Akitoa ufafanuzi kuhusu sababu za kutoa majibu hayo amesema “Baadhi ya maabara na famasi zimekuwa zikijiendesha kibiashara hivyo ni sababu mojawapo, mbili baadhi ya wagonjwa huwa hawaridhishwi na majibu ya kuambiwa kutokuwa na ugonjwa wowote.”

Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo, watalamu hao wamekuwa wakikosea na kwenda kinyume na taratibu za miongozo ya utoaji majibu ya malaria.

Aidha, amebainisha kuwa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na waratibu wa masuala ya afya ngazi ya halmashauri na Mikoa wamekuwa wakifanya ukaguzi wa aina hiyo ya wataalamu na wasimamizi wa maabara hizo ili kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu.

Chanzo: Habari Leo

Send this to a friend