
Raia mmoja wa Tanzania, Pinieli Vavai Lemomo, amekuwa miongoni mwa watuhumiwa watatu waliofikishwa katika Mahakama ya Machakos nchini Kenya kwa tuhuma za uporaji wa kutumia nguvu wa magari katika Barabara Kuu ya Nairobi-Mombasa.
Lemomo alikamatwa akiwa na wenzake wawili, Richard Otieno na Jane Muthui, muda mfupi baada ya tukio la utekaji wa gari lililoripotiwa na Polisi aina ya Range Rover. Inadaiwa kuwa watuhumiwa hao ni sehemu ya genge la kihalifu linalolenga magari ya kifahari.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, Lemomo hakuwa na hati yoyote ya utambulisho wakati wa kukamatwa, hali iliyowalazimu maafisa wa usalama kuwasiliana na shirika la kimataifa la upelelezi, Interpol, kwa ajili ya kubaini uraia wake halisi pamoja na historia ya uhalifu anaoweza kuwa nao katika mipaka ya kimataifa.
Aidha, upande wa mashtaka umewasilisha ombi la kuwashikilia kwa siku 15 zaidi ili kukamilisha uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma zinazowakabili.
Mahakama imeridhia ombi hilo na kuagiza washtakiwa waendelee kushikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Machakos hadi kesi yao itakapotajwa tena Juni 23, 2025.
