Mtanzania ateuliwa kuongoza Benki ya Dunia Cambodia

0
36

Benki ya Dunia (WB) imemteua Mtanzania, Maryam Salim kuwa mwakilishi wa benki hiyo (Country Manager) nchini Cambodia. Bi. Salim anachukua nafasi ya Inguna Dobraja, ambaye amehamishiwa Moldovia.

Bi. Salim ataongoza shughuli za siku kwa siku za Benki ya Dunia zinazohusisha serikali na wadau wamaendeleo, ikiwa ni pamoja na miradi yenye thamani ya US$1.1 bilioni, inayotekelezwa na wakala wa serikali ambapo WB inatoa msaada wa kiufundi. Miradi hiyo inaendana na mpango wa maendeleo wa Cambodia, ambapo benki hiyo ina malengo ya kuwezesha kupunguza umasikini na kuwezesha mafanikio shirikishi.

“Ni furaha kubwa sana kwangu kuchukua wadhifa huu mpya, na ninafurahia sana kurejea Cambodia  miaka 17 tangu nilipofanya kazi hapa kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa mfuko wa maendeleo ya jamii, unaolenga kuimarisha jamii na kupambana na umasikini.

“Nitashirikiana na watendaji wenzangu wa Cambodia kuiwezesha nchi kupambana na madhara yanayoendelea ya janga la COVID-19, kuweka mkakati wa kuinua uchumi, na kuweka misingi ya kukabiliana na matatizo mengine mbeleni,” amesema Bi. Salim (tafsiri ya mwandishi).

Bi. Salim ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 ndani ya Benki ya Dunia, ambapo kazi ya karibuni alikuwa Mwakilishi wa WB nchini Albania. Aidha, ameshika nyadhifa nyingine ndani ya benki hiyo Washington DC, nchini Marekani.

Mtanzania huyo ana shahada ya umahiri katika uchumi wa kimafaifa na uhusiano kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins na Udaktari wa Sheria (Juris Doctorate) kutoka Chuo Kikuu cha Georgetown, vyote vya Marekani.

Send this to a friend