Mtanzania mmoja atumie laini moja kwa mtandao mmoja- Naibu Waziri Ujenzi

0
13

Serikali imesema kuwa inatamani Mtanzania mmoja, atumie laini mmoja kwa mtandao mmoja na endapo mtu atahitaji laini ya pili katika mtandao huo huo (ambao tayari ana laini ya kwanza), basi atalazimika kutuma maombi maalum.

Hayo yamesemwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa kipindI cha maswali na majibu.

Naibu Waziri amelazimika kutoa ufafanuzi huo wakati akijbu swali la
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliyetaka kujua kama serikali haioni kuwa itakuwa ikiathiri mawasiliano miongoni mwa watu endapo itawataka kuwa na laini moja pekee ya simu.

Mhandisi Nditiye akaeleza kuwa, alichokisema hakimaanishi kuwa mtu atakuwa na laini moja pekee ya simu, bali atakuwa na laini moja kwa mtandao mmoja. Hii ina maana kuwa, utatakiwa kuwa na laini moja ya mtandao “X”, na kama utahitaji laini ya pili ya mtandao “X” basi utatuma maombi maalumu.

Lakini kwa mtu ambaye ana laini ya mtandao “X” ataweza kununua laini ya mtandao “Y” bila kutuma maombi hayo.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inakusudia kuondoa usumbufu na utapeli ambao wananchi wamekuwa wakikumbana nao, kutokana na uwepo wa laini nyingi zilizozagaa hovyo.

Aidha, ameongeza kuwa tayari wameyaandikia barua makampuni ya mawasiliano nchini kuyaeleza juu ya kusudio hilo.



Send this to a friend