Mtendaji wa Serikali adaiwa kumuua mkewe na kukaa naye ndani

0
74

Ofisa Mtendaji wa Serikali za Mitaa, Gongola Mboto, Dominic Mushi anadaiwa kumuua mke wake, Dayana Hugo (38) katika nyumba wanayoishi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Foka Dinya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo mtuhumiwa yuko chini ya ulinzi wa polisi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, baada ya kujaribu kujiua kwa sumu.

“Tulifika eneo la tukio na kumkuta mshitakiwa akiwa kwenye hali isiyo nzuri, alitaka kujiua kwa vidonge mbalimbali alivyokuwa tayari kameza na kuchanganya na pombe aina ya K-Vant na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana akiwa chini ya ulinzi na atakapopata nafuu atafikishwa mahakamani,” ameeleza.

Ameongeza kuwa “Katika mashahidi ndipo itathibitika kama aliua kwa kukusudia au la. Ushauri wangu kwa wanandoa, mnapokuwa na changamoto yoyote kaeni chini mzungumze.”

Akisimulia tukio hilo, baba wa Dayana, Damian Hugo amesema walipata wasiwasi baada ya kutomuona binti yao kanisani siku ya Jumatatu na ndipo mama yake alipoamua kumpigia simu ambayo ilipokelewa na mume wa marehemu na alipoulizwa kuhusu mkewe alisema amefariki tangu siku tatu zilizopita.

Baada ya kupewa taarifa hiyo, amesema walimtuma pacha wa marehemu aitwaye David ili kufuatilia jambo hilo na ndipo alipokuta mauaji hayo huku mtuhumiwa akiwa pembeni ya mwili huku akitokwa na povu mdomoni.

Polisi wanaendelea na chunguzi zaidi wa tukio hilo na mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa Rombo mkoani Kilimanjaro. Marehemu ameacha mtoto wa umri wa mwaka mmoja na miezi miwili.