Mtoto (13) auawa na kaka yake kisa ugomvi wa kifamilia

0
48

Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoani Morogoro, Rapha Meela amethibitisha kutokea kwa mauaji ya Faidhati Ibrahim Gadafi (13) mwanafunzi wa shule ya msingi Mwenge aliyeuawa kwa kukatwa mapanga na kaka yake, Shomari Malima, nyumbani kwao Tambukareli, Kata ya Kingolwila, Manispaa ya Morogoro, chanzo kikiwa ni ugomvi wa kifamilia.

Akizungumza msibani hapo, baba mzazi wa marehemu Ibrahim Gadafi ameeleza kuwa siku hiyo ya tukio  alikwenda kumfuata mkewe, wakati wakiwa njiani wakirejea nyumbani majira ya saa moja jioni, alipigiwa simu na shemeji yake akimtaarifu kuwa mtuhumiwa anafanya vurugu .

“Nilipigiwa simu na shemeji yangu anayeishi Dar es salaam akasema Shomari anamsumbua mama yake, nyumbani kwao na kwangu ni mbali, hivyo nilidhani hatoweza kufika. Baada ya kufanya vurugu akaja nyumbani na kuanza kumkata mapanga tukiwa bado hatujafika,” amesema.

Baada ya wazazi wake kuwasili nyumbani hapo, walikuta binti yao akiwa na hali mbaya na kuamua kumkimbiza hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, na ndipo mauti yalipomkuta Februari 15 mwaka huu.

Aidha, inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alitafutwa usiku mzima lakini hakupatikana, huku Jeshi la Polisi likiahidi kuendelea kufanya msako dhidi ya mtuhumiwa ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.

Hata hivyo inasadikika kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akimtishia mama yake mzazi kumuua akimtuhumu kwa uchawi.

Send this to a friend