Mtoto aharibiwa mkono kwa uzembe wa madaktari

0
41

Mtoto Nassoro Rashid (1) amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kutokana na kupata madhara ya kiafya ambayo wazazi wake wanadai kuwa ni uzembe wa madaktari na wauguzi wa hospoitali ya Tanzanite ya Jijini humo.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, mama wa mtoto, Neema Mohamed ameeleza kuwa Agosti 15, 2022 Nassoro alifikishwa katika hospitali ya Tanzanite na kugundulika kuwa ana malaria, kisha akatundikiwa dripu ya maji kwenye mkono wake wa kulia ambao baada ya muda ulionekana kuvimba na mtoto kupumua kwa shida.

“Nilitoa taarifa kwa madaktari, ndipo daktari mwingine tofauti na aliyetundika dripu alifika na kubaini maji yanaingia kwenye nyama badala yamshipa. Alirekebisha kasoro hiyo kwa kuichomoa sindano ya dripu na kuuhamishia mkono wa kushoto, lakini ule mkono wa kulia uliendelea kuvimba,” ameeleza Neema.

Ameongeza kuwa baada ya hali hiyo kuendelea ilimtia hofu na kuomba rufaa kwenda Bugando, lakini “uongozi wa hospitali ulidai tatizo tayari limerekebishwa, na baada ya kutishia kuripoti polisi ndipo uongozi ukakubali kutoa rufaa.”

Naye mmoja wa madaktari bingwa wa upasuaji katika hospitali ya Bugando (jina limehifadhiwa) amesema Nassoro atafanyiwa upasuaji mdogo wa kusawazisha majeraha hayo pamoja na upandikizaji wa nyama kwenye maeneo ya mkono yaliyolika.

Chanzo: Mwananchi