Mtoto asafiri zaidi ya 460km kwenye uvungu wa basi

0
24

Wasamaria wema mkoani Shinyanga wamemuokoa mtoto wa kike (13) aliyenusurika kifo baada ya kujificha chini ya uvungu wa basi akisafiri kutokea mkoani Kagera kuelekea Jijini Dar es Salaam kwa mama yake mzazi.

Inadaiwa majira ya saa 7 mchana, kampuni ya basi ya Frester lenye namba za usajili T 244 DWF wakati likifanyiwa ukaguzi na mafundi baada ya kufika wilayani Kahama mkoani humo, walimkuta mtoto huyo ambaye alikuwa akitokea Kijiji cha Kagya kwa baba yake mzazi aliyefahamiika kwa jina la Godfrey akielekea kwa mama yake Julietha Tofilo.

Akisimulia tukio hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Kahama, Abrahamani Nuru amesema baada kuokolewa, mtoto huyo alikabidhiwa katika ofisi za Ustawi wa Jamii, na baada ya mahojiano alikiri kuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kagya mkoani Kagera na aliamua kutoroka nyumbani kwenda kwa mama yake.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Manispaa ya Kahama, Flora Nangawe amewaomba madereva wa mabasi kufanya ukaguzi kwa kushirikiana na mafundi wao ili kuzuia matukio ya watoto wadogo wanaotumia mbinu hiyo.

Chanzo: Nipashe

Send this to a friend