Mtoto wa miaka 16 aiba mtoto wa miezi 9

0
62

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia binti mwenye umri wa miaka 16, aliyefahamika kwa jina la Maduki Sabuni mkazi wa Imalanguzo Ushirombo mkoani Geita kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa miezi 9 mkazi wa Manzese Manispaa ya Kahama.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP. Janeth Magomi amesema mtoto huyo aliibiwa wakati mama wa mtoto aitwaye Magdalena Sulas (23) akiendelea kufanya shughuli zake za biashara katika eneo la stendi ya magari yanayoelekea Kakola.

Amesema mara baada ya kupokea taarifa, Jeshi la Polisi lilianza upelelezi wa tukio hilo na kumkamata binti huyo akiwa na mtoto, na katika mahojiano ya awali mtuhumiwa alikiri kumuiba mtoto huyo.

“Mahojiano zaidi na mtuhumiwa yanaendelea na mtoto amepelekwa hospitali ya wilaya ya Kahama kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya kabla ya kukabidhiwa kwa mama yake, na mama yake mzazi amemtambua mtoto na alipoitwa jina na mama yake aliweza pia kumtambua mama yake na kumkimbilia,” ameeleza.

Aidha, Kamanda Magomi ametoa rai kwa viongozi katika ngazi za mitaa hususan wajumbe wa serikali za mitaa wawafahamu wakazi wanaoingia na kutoka katika mitaa yao ili kuweza kudhibiti wahalifu.

Send this to a friend