Mtoto wa Rais Museveni aunga mkono Urusi kuivamia Ukraine

0
38

Luteni Jenerali, Muhoozi Kainerugaba ambaye ni Mtoto wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ameunga mkono uamuzi wa Urusi kuivamia Ukraine, vita ambayo imeingia siku ya saba.

Kainerugaba ambaye ni Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Ardhini aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba watu wasio weupe wanaunga mkono hatua zilizochukuliwa na Urusi.

[Rais Vladmir] Putin yuko sahihi kabisa,”amesema Kainerugaba na kuongeza kuwa “Wakati Umoja wa Kisovieti (USSR) walipoweka silaha za nyuklia Cuba mwaka 1962, nchi za Magharibi zilikuwa tayari kuihatarisha dunia kwa ajili ya hilo. Sasa NATO inafanya hivyo hivyo na wanatarajia Urusi ifanye tofauti.”

Kainerugaba na Jenerali Mohamed Hamdan “Hemeti” wa Sudan wanatajwa kuwa maafisa pekee wa jeshi kutoka nchi za Afrika ambazo wametangaza wazi kuunga mkono uamuzi wa Urusi.

Mtoto huyo anadaiwa kuwa huenda akarithi kiti cha Urais wa Uganda kutoka kwa baba yake ambaye sasa ana umri wa miaka 77, na amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.

Send this to a friend