Mtoto wa Rais Yoweri Museveni atangaza kugombea Urais 2026

0
52

Mkuu wa zamani wa Jeshi la Ardhini la Uganda na mtoto wa kiume wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ameweka wazi nia yake ya kugombea Urais katika uchaguzi mkuu nchini humo utakaofanyika mwaka 2026.

Jenerali Muhoozi kupitia ukurasa wake wa Twitter ameweka ujumbe huo huku akidhihirisha kwamba ni majibu kwa wale waliokuwa wakihoji suala la yeye kugombea Urais.

“Katika jina la Yesu Kristo, kwa jina la vijana wa Uganda na dunia kwa ujumla na katika jina la mapinduzi makubwa, nitagombea Urais mwaka 2026,” ameandika Muhoozi akidai sio sawa kwa umri wake ambao anakaribia miaka 49 pasipokushika nafasi hiyo.

“Nani anakubaliana na mimi kwamba muda wetu vijana umewadia?, inatosha sasa kuendelea kuongozwa na wazee na kututawala, ni muda wa vijana kung’aa, Waziri Mkuu wa Uingereza ana miaka 42, Waziri Mkuu wa Finland ana miaka 37, sisi wengine tunakaribia miaka 50, tumechoka kusubiri, nitasimama kugombea,” amesisitiza.

Send this to a friend