Mtu mmoja amefariki na askari mmoja kujeruhiwa wakati Jeshi la Polisi likiwazuia wananchi ambao lengo lao lilikuwa kuingia ndani ya mgodi wa Barrick North Mara kwa lengo la kufanya uhalifu.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya imesema askari hao walikuwa wakifanya doria katika mgodi huo ndipo wananchi hao walipowashambulia kwa mawe na silaha za jadi kwa muda wa takribani nusu saa.
“Askari walifanikiwa kuwadhibiti na kutawanyika. Katika vurugu hizo ilibainika Emmanuel Nyakoringa (36), mkulima na mkazi wa kijiji cha Kewanja amejeruhiwa na kitu chenye ncha kali na kupelekea kupoteza maisha. Aidha, askari mmoja alijeruhiwa na anaendelea na matibabu,” imeeleza taarifa ya Polisi.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa watu wote waliohusika na uvamizi huo.
Vilevile, jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya uhalifu hususani uvamizi wa migodi na kuwataka kutii sheria bila shuruti.