Mtuhumiwa wa mauaji wa kukodi auawa na polisi

0
18

Mtuhumimiwa wa mauaji ya kukodiwa, Heleni Nyankole maarufu Beberu (36), Mkazi wa Kijiji cha Kapanga wilayani Tanganyika ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kutokea mabishano na askari hao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Ally Makame amesema mtuhumiwa huyo aliuawa usiku wa kuamkia jana wakati akipambana na polisi.

Kamanda amefafanua kwamba Juni 28, mwaka huu mtuhumiwa alikodiwa na watu wawili wakazi wa Kijiji cha Luhita- Bujombe kwa makabuliano ya kumlipa TZS 800,000 ili amuue mwanakijiji aliyejulikana kwa jina Mandalu Ndulu (36) na mtuhumiwa alitekeleza mauaji hayo kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni.

Amesema polisi baada ya kupata taarifa za tukio hilo waliwakamata watuhumiwa hao wawili na baada ya kuwahoji walikiri kumkodi mtuhumiwa huyo ambapo walimpa TZS 300,000 ikiwa ni malipo ya awali kisha kutekeleza mauaji hayo.

“Tulianza msako mkali Julai 7, 2022 usiku tulimkamata  mtuhumiwa huyo wa mauaji kijiji cha Lwega wilayani Tanganyika akiwa amelala ndani ya nyumba yake, polisi walipomuamuru kujisalimisha alikaidi na kupanda juu ya dari kisha kutoboa paa la nyumba iliyoezekwa kwa nyasi kwa kutumia panga, akiwa juu alijaribu kushuka, ghafla alishuka akiwa na kipande cha nondo kwa lengo la kumjeruhi askari” amesema.

Aidha Kamanda Makame amesema kuwa askari walifyatua risasi hewani ili kumuonya lakini alikaidi na kuendelea kuwafuata hivyo walifyatua risasi nyingine iliyomjeruhi tumboni na kupelekea kupoteza maisha alipokuwa akikimbizwa katika kituo cha afya.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mauaji ndani ya Mkoa wa Katavi na nje ya mkoa huo.

Send this to a friend