
Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili imefafanua kuwa watu wanaoruhusiwa kuchangia figo ni ndugu wa karibu wa mgonjwa pekee, na uchangiaji huo hufanyika bila malipo.
Taarifa hiyo imetolewa kufuatiwa taarifa zinazojirudia zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu utaratibu wa kuchangia kwa wagonjwa wenye uhitaji huo, huku hospitali hiyo ikieleza kuwa tangu huduma hiyo ianze kutolewa rasmi Septemba 2017, hadi sasa wagonjwa 106 wameshanufaika.
“Hospitali inatumia kanuni za Huduma za Figo zilizoandaliwa mwaka 2017 kwa kuzingatia miongozo na maazimio ya kimataifa na kuidhinishwa na Wizara ya Afya kabla ya kuanza huduma hizo. Ikumbukwe kuwa miongozo na maazimio ya kimataifa vinakataza biashara ya uuzaji viungo vya binadamu,” imeeleza taarifa.
Imeongeza kuwa hospitali ina kamati maalumu ya kuidhinisha mgonjwa kufanyiwa upandikizaji inayojumuisha wanasheria, viongozi wa dini, madaktari na maafisa ustawi wa jamii, ambayo hupitia maombi yote ya upandikizaji figo kwa kufanya ukaguzi wa nyaraka za uthibitisho wa uhusiano wa damu kati ya mgonjwa na mchangiaji ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, picha pamoja na majibu ya vipimo vya maabara.







