Muigizaji Jimmy Mafufu Aingilia Kati Sakata la Martha Karua, Aonya Wakenya Kuheshimu Mipaka ya Tanzania

0
2

Muigizaji maarufu wa filamu nchini Tanzania, Jimmy Mafufu, amevunja ukimya wake kuhusu tukio lililomhusisha mwanasiasa mashuhuri wa Kenya, Martha Karua, ambaye alidai kuzuiwa kuingia nchini Tanzania na kurejeshwa kwao mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari, Mafufu amesema kitendo cha Bi. Karua kulalamikia hatua ya vyombo vya dola vya Tanzania ni ishara ya kutoelewa taratibu za kidiplomasia na za kiutawala zinazolinda mamlaka ya nchi huru. Alisisitiza kuwa Tanzania ni taifa lenye miongozo na sheria zake, ambazo hazipaswi kuingiliwa na watu kutoka nje, hata kama ni kwa kisingizio cha haki za binadamu au harakati za kisiasa.

“Si jambo la busara kwa mwanasiasa kutoka taifa jirani kuja kuhoji taratibu za kiusalama za nchi yetu. Tanzania si koloni, ni nchi huru yenye misingi na taratibu zake. Martha Karua na wenzake wanapaswa kuheshimu hilo,” alisema Mafufu kwa msisitizo.

Mafufu pia alionya baadhi ya Watanzania ambao, kwa maoni yake, wamekuwa wakishabikia au kuunga mkono kila jambo linalotolewa na viongozi wa nje, hata kama linakwenda kinyume na maslahi ya kitaifa. Alitoa wito kwa Watanzania kuweka mbele uzalendo na kuheshimu vyombo vya usalama vya taifa.

Hata hivyo, suala hili limezua mijadala mitandaoni ambapo baadhi ya watu wamepongeza hatua ya Tanzania, huku wengine wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu sababu halisi za kurejeshwa kwa Martha Karua. Hadi sasa, serikali ya Tanzania haijatoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.

Send this to a friend