
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limesema mwanamke aitwaye Maria Salavatory ameuawa baada ya kupigwa na kitu butu kichwani na kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili na mume wake aitwaye Mayala Juma, katika Kitongoji cha Bugoma, Kijiji cha Kilombero Wilaya ya Geita.
Taarifa ya Polisi imeeleza kuwa baada ya mwanaume huyo kufanya mauaji alijifungia chumbani na kunywa sumu aina ya synom crown pamoja na dawa nyingine ili kujiondoa uhai. Hata hivyo alikimbizwa hospitali ya Wilaya ya Geita ili kuokoa maisha yake, lakini alfajiri ya Novemba 18, 2025 alifariki dunia.
Jeshi la Polisi limesema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, baada ya mume kumtuhumu mkewe kuwa na mahusiano na wanaume wengine.
Miili ya wanandoa hao tayari imekabidhiwa kwa ndugu tayari kwa ajili ya mazishi.








