Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amekanusha ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia, ambayo iliitaja nchi ya Uganda kuwa bado ni taifa la kipato cha chini.
Julai 1, mwaka huu benki hiyo ilitoa ripoti kuwa pato la taifa la Uganda kwa kila mtu lilifikia $840 (TZS milioni 1.95) kwa mwaka, kulingana na taarifa ya kipindi kilichopita cha mwaka 2020/21.
“Uchumi unakua, juzi nilikuwa na mabishano kuhusu kama tumeenda kwenye kipato cha kati au la, tunathibitisha tena, sijui Benki ya Dunia inapata wapi data zao,” amesema.
Tangazo la nafasi za kazi 171 Serikalini
Ameongeza; “Lakini takwimu zetu kuhusu nchi yetu ni kwamba, sasa tuko kwenye pato la Taifa (Gross Domestic Product) kwa kila mtu dola 1,046 (TZS milioni 2.43) na hiyo tayari iko kwenye kipato cha kati. Tunahitaji kukaa huko kwa miaka mitatu zaidi au kwenda juu ili kutangazwa rasmi. Tuna pesa na mambo ya kufanya ni mengi, ndio maana kuweka vipaumbele inakuwa muhimu.”
Aidha, wakati wa hotuba ya hali ya Taifa mwezi Juni, Rais Museveni alitangaza kwamba Uganda ilikuwa imefikia katika uchumi wa kati.