Muswada Kenya wapendekeza kifungo cha mwaka mmoja kuandamana bila taarifa

0
155

Kenya imewasilisha muswada mpya wa mwaka 2024 unaolenga kudhibiti mikusanyiko na maandamano ya umma, huku ukiweka masharti makali kwa waandaaji na washiriki wa maandamano yasiyo na kibali.

Muswada huo wa Mikutano na Maandamano wa mwaka 2024 uliowasilishwa na Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, unapendekeza kifungo cha hadi mwaka mmoja jela au faini ya KSh 100,000 [TZS milioni 2] kwa mtu yeyote atakayeshiriki maandamano ya ghafla bila kutoa taarifa kwa mamlaka.

Kwa mujibu wa muswada huo, waandaaji wa maandamano wanatakiwa kutoa taarifa kwa polisi kati ya siku 3 hadi 14 kabla ya maandamano kufanyika. Taarifa hiyo lazima ijumuishe jina kamili la mwandaaji, anwani, tarehe na saa ya maandamano, eneo na njia yatakayotumika, idadi ya washiriki wanaotarajiwa, pamoja na kaulimbiu au mabango yatakayotumika.

Aidha, afisa msimamizi wa maandamano atakuwa na mamlaka ya kuweka masharti au vikwazo kwa maandamano yoyote, iwapo itaonekana kuwa kuna tishio kwa usalama wa umma au ukiukwaji wa haki za wengine. Pia mwandaaji atawajibika kwa hasara au uharibifu wowote wa mali utakaojitokeza wakati wa maandamano hayo.

Rais William Ruto tayari ametangaza kuwa atashirikiana na Bunge na Idara ya Mahakama kuhakikisha sheria mpya inapitishwa ili kudhibiti maandamano na kulinda amani.

“Tutafanya mazungumzo na mahakama na wabunge. Nafikiri umefika wakati wa kuwa na sheria itakayosimamia namna tunavyoandamana nchini Kenya,” amesema Rais Ruto.

Send this to a friend