Muswada mpya wapendekeza faini ya TZS milioni 104 kwa wanaotumia miujiza kuwatapeli wananchi

0
83

Kiongozi yeyote wa kidini atakayefanya miujiza, uponyaji au baraka kwa njia ya udanganyifu kwa lengo la kuwaibia Wakenya wasio na hatia, atakabiliwa na hatia ya kutenda kosa na kulipa faini ya ya Ksh. 5 milioni [TZS milioni 104.7] au kifungo cha miaka kumi gerezani au vyote viwili endapo mapendekezo ya kikosi kazi kilichoundwa na Rais William Ruto yatakubaliwa.

Kikosi kazi hicho kilichojulikana kama Kikosi Kazi cha Rais kuhusu Mapitio ya Mfumo wa Kisheria na Udhibiti wa Mashirika ya Kidini nchini Kenya, kimewasilisha mapendekezo ya kutoa ufafanuzi juu ya jinsi taasisi za kidini zitakavyosimamiwa.

Mapendekezo hayo yamejumuishwa katika Muswada wa Mashirika ya Kidini wa mwaka 2024, ambapo moja ya mikakati iliyopendekezwa ni kuwafuatilia viongozi wa dini wanaowaomba waumini wao kutoa pesa ili kufanikiwa kifedha au kupata baraka kutoka kwa Mungu.

“Kiongozi wa kidini ambaye kwa njia ya uwasilishaji wowote wa uwongo na ulaghai, hila au njama za uponyaji, miujiza, baraka au maombi, anawaibia au kupata faida yoyote ya kifedha au manufaa ya kimwili kutoka kwa mtu yeyote au kumshawishi mtu huyo kupeleka fedha au mali kwa kiongozi wa kidini, anatenda kosa na akipatikana na hatia atawajibika kulipa faini isiyozidi Ksh.5 milioni au kifungo kisichozidi miaka kumi au vyote kwa pamoja,” inasomeka sehemu ya muswada huo

Aidha, muswada huo umeeleza kuwa kiongozi yeyote wa dini atakayetumia nguvu au vitisho vya kuwalazimisha watu kujiunga na dini yao atatozwa faini isiyozidi Ksh.1 milioni [TZS milioni 20.9] au kifungo cha miaka mitatu gerezani au vyote viwili.

Kwa upande mwingine, mtu yeyote atakayetumia dini kudharau imani ya dini ya mtu mwingine na kufanya jambo lolote linalotishia usalama wao atatozwa faini ya Ksh.5 milioni [TZS milioni 104.7], kifungo cha miaka 20 gerezani au vyote viwili.

Kikosi kazi hicho pia kilipendekeza kuwa makanisa hayapaswi kushiriki katika siasa ili kupata madaraka au kuandaa mjadala wa kumuunga mkono mgombea wa kisiasa, na iwapo yatapatikana na hatia, taasisi hiyo itawajibika kulipa faini isiyozidi Ksh.500,000 [TZS milioni 10.5] au kifungo cha miezi 6 gerezani au vyote viwili.

Send this to a friend