Mwajiri amchoma moto mfanyakazi wake wa ndani kwa kumwibia pesa

0
61

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia Christina Shiriri (43) maarufu kama Manka kwa tuhuma za kumuunguza moto mfanyakazi wake wa ndani, Grace Joseph (17) kwa kumwibia TZS 161,000.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Usagara wilayani Misungwi anatuhumiwa kumwagia mafuta mwilini kisha kumchoma moto mfanyakazi wake ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyalwigo wilayani humo mkoani Mwanza.

Kamanda Mutafungwa amesema binti huyo alifanyiwa ukatili huo Juni 04 mwaka huu saa nane usiku baada ya mwajiri wake kudai kuibiwa fedha hizo alizodai kuzihifadhi chumbani kwake na alipomuuliza Grace alikiri kuzichukua na alimrejeshea.

“Baada ya kurejeshewa fedha hizo, Christina Shiriri aliamua kumfanyia ukatili binti huyo kwa kumchoma moto mikono yote miwili, tumboni pamoja na mapaja yake yote mawili,” amesema Kamanda.

Aidha, amesema binti huyo alifikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya matibabu huku mtuhumiwa akishikiliwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Send this to a friend